MVUA MKUBWA ILIYONYESHA LEO JIJINI DAR YALETA USUMBUFU WA HALI YA JUU KWA WAKAZI WA KIMARA KILUNGURE MARA BAADA YA DARAJA KUFUNIKWA NA MAJI


Wakazi wa Kimara Kilungure wakiwa wametaharuki baada ya kukosa jinsi ya kuvuka daraja ambalo limefunikwa na maji yaliyosababishwa na Mvua Kali iliyonyesha leo Katika Jiji la Dar na kupelekea kuleta adha kwa watumiaji wa barabara hiyo huko Kimara Kilungure
Daraja lililopo Kimara kilungure likiwa limefunikwa na maji yaliyosababishwa na Mvua Kali iliyonyesha Jijini Dar mapema leo na kupelekea kuleta adha kwa watumiaji wa barabara hiyo na daraja huku wakazi maeneo hayo wakiwa wamesimama kwa kushindwa kuvuka kwa kuogopa kupoteza mali pamoja na maisha yao kutokana na maji kufunika daraja.

WANAWAKE WAKIRI KUFANYA NGONO KINYUME NA MAUMBILE: UTAFITI MONDAY, DECEMBER 17, 2012

Mtafiti Mwanasayansi Irine Mremi, kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadamu nchini Tanzania (NIMR) ambaye aliwasilisha ripoti hiyo kwa niaba ya watafiti wenzake wa NIMR. 
***
BAADHI ya wanawake kutoka katika Wilaya za Kinondoni, Tanga, Makete na Siha, wamekiri kufanya ngono kinyume na maumbile.


Hayo yalielezwa na Mtafiti Mwanasayansi Irine Mremi kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadamu nchini Tanzania (NIMR) wakati akiwasilisha utafiti uliofanywa na watafiti wa NIMR juu ya ufanyaji Ngono kinyume na maumbile katika kueneza maambukizi ya VVU/Ukimwi nchini na kuwasilishwa mbele ya Wanahabari na Watafiti jijini Dar es Salaam hivi karibuni.


Mremi amesema wanawake hao wamesema chanzo kikubwa kinacho wapelekea kufanya ngono kinyume na maumbile ni kujipatia kipato zaidi, Kuogopa kupata Mimba, kulinda usichana wao na baadhi ya mila na tamaduni za baadhi ya makabila.


“ Utafiti wetu uliwahusisha wasichana na wanawake wa rika kuanzia miaka 15 na kuendelea na kada tofauti katika jamii kama wanafunzi, wafanyakazi, wahudumu bar, wauguzi, makahaba na akina mama wa nyumbani, katika maeneo hayo watu 903 walijitokeza wakiwepo pia wanaume ambao wal;ihusishwa katika utafiti huo,” alisema Mtafiri Irine.


Aidha alisema wakati wa utafiti huo wanawake 44 kati ya 166 waliohojiwa walisema kuwa wanafanya tendo la kujamiiana kinyume na maumbile ambayo ni sawa na 26.5% huku 76.4% ya waliohojiwa walidai kufanhamu njia hiyo ya kufanya mapenzi.


Wilayani Tanga ndio kumeonesha kukithiri kwa vitendo vya wanawake kufanya mapenzi kinyume na maumbe na wanaume kuwafanyia wanawake kinyume na maumbile ukilinganisha na Makete ambako bado kuna idadi ndogo.


Wanaume waliohojiwa katika utafiti huo wamedai wao wanafanya kwa mtindo huo kwaajili ya kupata raha tu na imani ya kuwa huko hakuna maambukizi ya VVU/UKIMWI na wamekua wakitumia mafuta ya aina mbalimbali ilhali matumizi ya mipira ikiwa ni hafifu kwani wakitumia mipira wamedai kupunguza raha wanayo ipata.


Wanawake pia wamedai baadhi ya tamaduni zao hasa maeneo ya Mwambao huko Tanga msichana kuolewa na kukutwa usichana wake haupo (Bikira) ni aibu kwake na wazazi hivyo hulazimika kufanya mapenzi kinyume na maumbile, huku suala la Mimba nalo likichukua nafasi.


Watafiti hao wamesema ufanyaji huo wa ngono kinyume na maumbile umekuwa ukisababisha michubuko kirahisi na kuchangia maambukizi ya Ukimwi kwa kasi tofauti na kutumia njia ya kawaida ya kujamiiana.


Aidha imedaiwa kuwa wanawake wengi wanaofanya ngono kinyume na maumbile wamekuwa wakipata shida wakati wa kujifungua kwa misuli yao ya kushindwa kuhimili kusukuma mtoto, jambo ambalo limekuwa likileta tabu kwa wahudumu wa Afya hasa wakunga ambao ni wachache mahospitalini kutumia muda mrefu kumhudumia mjazito mmoja huku wengine wakiendelea kuteseka wodini wakati wa kujifungua.


Watafiti hao wameshauri elimu zaidi ya kujikinga na maambukizi ya ukimwi na njia salama za kujamiiana kufundishwa mashuleni ili kuondoa dhana ya kujamiiana kinyume na maumbile kuwa haiambukizi virusi vya Ukimwi.


Watafiti walioshiriki katika utafiti huo ni pamoja na Akili kalinga, Elizabeth H Shayo, Irene Mremi , Godlisten materu, Stella Kilima, Gibson Kagaruki, Anjela Shija, Judith Msovela, Dk. Leornad Mboera, Dk.Julius Massaga, Kesheni Senkoro na Basiliana Emid wote kutoka NIMR.

TAARIFA RASMI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA JAMHURI YA WATU WA CHINA, MHE. XI JINPING NCHINI, TAREHE 24 – 25 MACHI 2013 ILIYOTOLEWA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, MHE. BERNARD K. MEMBE (MB), TAREHE 22 MACHI 2013



1.0     UTANGULIZI
1.1     Ndugu waandishi, nimewaita leo ili kuwaeleza kuhusu ziara ya kihistoria hapa nchini ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping ambayo itafanyika hivi karibuni. Najua mtakuwa mmekwishasikia kuwa Rais huyu atafika nchini hivi karibuni.
Sasa niwatangazie rasmi kuwa taarifa hii ni sahihi na ziara hiyo itafanyika tarehe 24 – 25 Machi, 2013. Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais Xi barani Afrika mara tu baada ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo ya Urais mnamo tarehe 14 Machi, 2013.
1.2     Mahusiano  ya  Tanzania na China yametoka mbali, tangu enzi ya waanzilishi wa mataifa haya mawili, yaani Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mao Zedong  wa China. Ifahamike kuwa, kutokana na mahusiano haya ndipo mmoja ya miradi mikubwa kabisa iliyofanywa na China barani Afrika ulitokea. Mradi huu ni reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA). Pamoja na kuwa mradi wa kimaendeleo, reli hii ya TAZARA ilitusaidia katika ukombozi wa bara la Afrika – kama moja ya njia za usafiri, hivyo kuifanya China kuwa rafiki wa kweli. Mradi mwingine mkubwa ni ujenzi wa jengo la Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia. Haya, kati ya mengineyo, yanafanya ugeni huu kuwa wa kihistoria na heshima kubwa kwetu.
1.3    Rais Xi anakuja kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na akiwa nchini atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Kikwete, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein. Mheshimiwa Xi ataambatana na mke wake, pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali ya China wasiopungua 25.
2.0     RATIBA YA MGENI KWA KIFUPI
2.1     Rais Xi Jinping atawasili nchini siku ya jumapili tarehe 24 Machi, 2013 saa 10:25 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege maalumu aina ya Boeing 747 ambapo atalakiwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
2.2     Baadaye Rais Xi pamoja na ujumbe wake watafanya mazungumzo rasmi na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazungumzo hayo yataanza saa 12:15 jioni na yatafanyikia Ikulu.
2.3     Baada ya mazungumzo rasmi, Rais Xi pamoja na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete watashuhudia utiaji saini wa Makubaliano na Mikataba mbalimbali (kumi na tisa) ya ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania/na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa upande mmoja na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa upande mwingine. Kwa kifupi mikataba hiyo inahusu kukuza uwekezaji na biashara baina ya nchini za Tanzania na China, kukuza ushirikiano wa kiutamaduni baina ya nchi hizi mbili na watu wake, nk.
2.4     Baada ya tukio hilo, Rais Xi pamoja na ujumbe wake watahudhuria dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa  kwa heshima yake na Rais Jakaya Kikwete. Dhifa hiyo itafanyika Ikulu kuanzia saa 1:40 usiku. Hilo ndilo litakuwa tukio la mwisho kwa siku ya kwanza.
2.5     Siku itakayofuata ya tarehe 25 Machi, 2013 saa 3:10 asubuhi Rais Xi atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Ali Mohamed Shein pamoja na ujumbe wa Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
2.6     Tukio litakalofuata litakuwa ni uzinduzi na makabidhiano rasmi ya kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere. Baada ya makabidhiano ndipo Rais Xi atatoa hotuba maalumu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. Hotuba hiyo itajikita katika kuelezea Sera ya Serikali mpya ya China kwa bara la Afrika. Watu kutoka kada mbalimbali kama vile Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, Wanafunzi, Wabunge, Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Serikali, Wafanyabiashara, n.k. wamealikwa kuhudhuria ukumbini hapo.
2.7     Mchana wa tarehe 25 Machi, 2013 Rais Xi Jinping ataelekea katika Makaburi ya Wataalamu wa Kichina ya Majohe yaliyopo katika kijiji cha Majohe – Ukonga ambapo atatoa heshima zake kwa Wachina waliofariki wakati wakijenga Reli ya TAZARA.
2.8     Baada ya hapo Rais Xi ataelekea Uwanja wa Ndege wa Julius K. Nyerere ambapo ataondoka saa 10:40 jioni kuelekea nchini Afrika Kusini kuhudhuria Mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi za BRICS.
3.0     FAIDA ILIYOPATA TANZANIA KUTOKANA NA UHUSIANO NA CHINA
3.1     Jambo kubwa Tanzania inalojivunia tangu kuanzisha uhusiano na China ni kukua kwa urafiki wa karibu sana na China;  urafiki wa kuaminiana na kusaidiana katika nyanja mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa. Uhusiano huo wa karibu unazidi kukua kila kukicha.
3.2     Kwa upande wa ushirikiano wa kiuchumi Tanzania inajivunia miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyotekelezwa kwa ushirikiano na China. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na:
i. Mradi wa Reli ya TAZARA – kama nilivyoeleza hapo awali Mradi huu umekuwa mhimili na kiungo muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa Tanzania na nchi jirani za Zambia, DRC, Zimbabwe n.k, hususan  katika sekta ya usafirishaji wa rasilimali ghafi, bidhaa za kibiashara na abiria
ii. Kiwanda cha nguo cha URAFIKI – (licha ya changamoto kadhaa zinazokikabili) kiwanda hiki kimetoa ajira kwa Watanzania wengi, pamoja na soko kwa pamba inayolimwa hapa nchini.
iii. Miradi mikubwa ya maji ya Shinyanga, Dar es Salaam na Pwani.
iv. Viwanja vya kisasa vya michezo – Uwanja wa Taifa (Dar es Salaam) na Karume Stadium (Zanzibar).
v. Kituo cha maonesho na majaribio ya zana za kilimo cha Mvomero, Morogoro.
vi. Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius K. Nyerere. Manufaa ya Kituo hiki cha Mikutano ni kama yale yanayopatikana katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
vii. Mradi wa ujenzi wa mkongo wa Taifa kwa Tanzania bara na Zanzibar – mradi huu ni muhimu sana katika maendeleo ya sekta ya Teknohama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano). Manufaa yake yatapatikana si tu hapa Tanzania lakini pia kwa nchi za jirani kama vile Rwanda, Burundi, n.k, kwani huduma hii itatolewa kibiashara.
viii. Mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam – Mradi huu utakapokamilika hapo mwakani utatupatia uhakika wa umeme, pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama zake. Pia utapelekea kupungua kwa gharama za maisha kwa ujumla na kukua kwa kipato cha mtu mmoja mmoja kiuchumi.
ix. Manufaa mengine mengi yanatarajiwa kupatikana mara baada ya ziara.
4.0 MATARAJIO YA TANZANIA KUTOKANA NA ZIARA HII
4.1     Katika ziara hii ya kihistoria Tanzania inatarajia kufaidika kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo:
i. Kufungua milango ya uwekezaji katika sekta mbalimbali. Ziara hii inafuatiliwa na kumulikwa na nchi karibu zote duniani; pamoja na makampuni makubwa kila kona ya dunia. Ziara ya Rais wa huyu wa China inatuma ujumbe kwa wawekezaji kote duniani kuhusu mazingira mazuri na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.
ii. Wakati wa ziara hii mikataba na makubaliano zaidi ya 19 yatatiwa saini kati ya Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande mmoja, na Serikali ya China kwa upande mwingine (tafadhali rejea kiambatisho Na.1 kwa orodha ya Makubaliano na Mikataba iyakayotiwa saini.)
Kama ilivyoelezwa hapo awali, Mikataba na makubaliano haya yanagusa sekta za kilimo kibiashara, uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu, miradi ya maji na umeme, fursa za kimasomo kwa vijana wa Kitanzania nchini China, nk.
5.0     HITIMISHO
5.1     Uhusiano kati ya Tanzania na China ni wa muda mrefu tangu miaka ya 1950 wakati bado Tanzania (Tanganyika kwa wakati huo) ikiwa katika harakati za kupigania Uhuru. Mwaka kesho (2014) nchi zetu mbili zitasherehekea miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia. Uhusiano huu unatoa picha ya ukaribu uliopo kati ya Serikali za nchi za Tanzania na China pamoja na watu wake.
5.2     Hivyo basi, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Watanzania wote kwa ujumla tujitokeze kwa wingi kumlaki Rais Xi Jinping atakapokuwa anawasili kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere mpaka Hoteli ya Serena atakapofikia kwa kupitia Barabara ya Pugu/Julius K. Nyerere.
Rais wa China, Xi Jinping 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ziara ya kitaifa ya siku mbili ya Rais mpya wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping atakayoifanya hapa nchini kuanzia tarehe 24 hadi 25 Machi, 2013. Wengine katika picha ni Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) (kulia), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Bw. John Haule, Katibu Mkuu wa Wizara  wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Membe, Mhe. Maalim, Bw. Haule na Balozi Gamaha wakisikiliza swali kutoka kwa Mwandishi wa Habari (hayupo pichani) wakati wa mkutano kuhusu ziara ya Rais wa China, Mhe. Xi Jinping hapa nchini.
Mmoja wa waandishi wa habari kutoka China akiuliza swali kwa Mhe. Membe (hayupo pichani) wakati wa mkutano kuhusu ziara ya Rais wa China hapa nchini
Waandishi kutoka mashirika mbalimbali ya habari ya China pia walikuwepo kwenye mkutano huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajab Gamaha (kulia) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Philip Marmo (katikati) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Bertha Semu-Somi wakimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani) alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais wa China hapa nchini. Picha kwa hisani ya Haki Ngowi
---

MAANDAMANO YA CHADEMA KESHO: MBOWE ADAI YAKO PALE PALE NA WATAANDAMANA MBELE YA RAIS WA CHINA



LICHA ya serikali kuyapiga marufuku maandamano yaliyoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuishinikiza kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Naibu wake wajiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne 2012, chama hicho kimesema yapo pale pale.

Chama hicho kimewaomba wananchi wote waliochoshwa na kufelishwa kwa watoto wao, kunyimwa elimu bora wajitokeze kuandamana kwa nguvu zote, na wanafunzi wote waliofeli pia wajitokeze kudai elimu bora kwani ni haki yao. 

Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana na kutoa msimamo huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema “wananchi wajitokeze kwa wingi ili kilio chao kisikike duniani kote.” 

Alisisitiza kuwa maandamano hayo yatafanyika mbele ya ugeni wa Rais wa China, Xi Jinping ili kufikisha kilio hicho na kamwe haikubaliani na sababu ya serikali kuyazuia kwa sababu ya ugeni huo. 

Alisema maandamano hayo yatasaidia kupuuza kunakofanywa na Serikali ya CCM kuonwe na dunia nzima maana vyombo vyote vya habari vitafuatilia tukio hilo. 

Mbowe aliongeza kuwa, “Watanzania waliochoshwa na ubabaishaji katika elimu wajitokeze, kulaani kitendo cha Waziri Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo kulindwa na serikali, badala ya kuwajibishwa kwa matokeo mabaya ya watoto wa Kitanzania.” 

Alipoulizwa itakuwaje maana kutakuwa na ugeni wa Rais wa China nchini, sababu ambayo hata serikali imeitumia ili kuyazuia maandamano hayo, Mbowe alijibu: “Kilio chetu hakikuja na Rais wa China, kama Serikali ya CCM wanaona aibu kumwajibisha waziri mmoja na naibu wake, basi wasubiri aibu ya dunia kuona jinsi Tanzania inavyoendeshwa kibabe, ikiwa haina elimu bora. 

“Tumetangaza maandamano wiki tatu zilizopita, hatukuwa na taarifa na ujio wa Rais wa China, lakini jinsi Mungu alivyo upande wetu amemleta Rais wa China, kweli Mungu ni mwema, hakuna tena nafasi ya kusubiri kuficha ubovu katika sekta ya elimu nchini, ndani ya siku ambayo CHADEMA waliandaa maandamano ili dunia nzima isikie kilio cha Watanzania kuhusu elimu. 

“Sababu kuwa CCM nao wameandaa maandamano kupinga maandamano ya CHADEMA hazina msingi ni kutowajibika kwa Jeshi la Polisi. Hatukatazi maandamano, polisi wapange ratiba siku tofauti, sisi tutaandamana kumpinga waziri ili kama CCM wataandamana kumpongeza waziri wao wapangiwe siku yao, ila sisi tulitangaza mapema na barua tulipeleka kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.” 

Alipoulizwa kwanini asisubiri Tume ya Waziri Mkuu itoe majibu, Mbowe alisema: “Hatuna shida na Tume ya Waziri Mkuu, matatizo ya elimu katika nchi yetu yapo wazi, tukizungumza bungeni wanatuchakachua, na sasa huku nje wanatukejeli, tunataka ifike mahali wajue kuwa nchi hii ni yetu sote, na Watanzania wanapaswa kusikilizwa kilio chao.” 

Kwa mujibu wa Mbowe, maandalizi ya maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam, yamekamilika. 

Jana, Idara ya Habari (Maelezo) ilitoa barua iliyosainiwa na mkurugenzi wake, Assah Mwambene kuzuia maandamano yaliyokuwa yafanyike Jumatatu ijayo katika mikoa ya Mbeya na Arusha tu. 

Taarifa hiyo haikuzungumzia maandamano yaliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam wala Mwanza. 

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, serikali ilisema kuwa maandamano ya CHADEMA yalipangwa kuhusisha wananchama kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma, na kuongeza kuwa CCM ilipanga kufanya maandamanno yake mkoani Arusha kupinga kusudio la CHADEMA kuandamana, wakieleza kwamba wana imani na tume maalumu ya Waziri Mkuu inayochunguza tatizo la kufanya vibaya wanafunzi wa kidato cha nne. 

Awali CHADEMA walitangaza maandamano yatakayofanyika katika kanda nne. Kanda ya Kusini yatafanyika Mbeya; Kanda ya Ziwa yatafanyika Mwanza; Kanda ya Kaskazini yatafanyika Arusha, na Kanda ya Mashariki yatafanyika Dar es Salaam. 

Tanzania Daima ilipomuuliza Mkurugenzi wa Maelezo imekuwaje yeye akawa msemaji wa jambo hili, alijibu: “Mimi ni msemaji wa serikali, hata Ikulu naisemea, hivyo usiulize kwanini naisemea polisi.” 

Sababu nyingine iliyotolewa na serikali kupitia Maelezo ilisema ni kwa sababu siku hiyo ni muhimu kwa Watanzania kumpokea Rais mpya wa China ambaye atakuwa na ziara ya siku mbili nchini. 

Februari 19 mwaka huu akiwa jijini Mwanza, Mbowe alitoa siku 14 kwa Waziri Kawambwa kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne. 

Kauli hiyo ilitolewa siku moja baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 ambapo asilimia sitini ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wamefeli. 

Gazeti la- Tanzania Daima

WALIKI MAARUFU WA MAWALLA ADVOCATES AFARIKI DUNIA KWA KUJIUA


Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la Mwananchi, ARUSHA-- Giza limeukumba Mkoa wa Arusha baada ya kutokea vifo vya ghafla vya watu maarufu. Jana Wakili Nyaga Mawalla alifariki baada ya kujirusha kutoka ghorofani akiwa jijini Nairobi, Kenya alikokwenda kwa matibabu.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa Nyaga alikufa baada ya kujirusha kutoka katika jengo la ghorofa ya hospitali aliyokuwa akitibiwa jijini Nairobi usiku wa kuamkia jana.

Mfanyakazi wa Kampuni ya Mawalla Advocate, John Minja aliliambia gazeti hili kuwa mwili wa marehemu ulitarajiwa kurejeshwa nchini jana.

“Hali yake haikuwa mbaya, kwani juzi mchana tulizungumza naye tukitaka kwenda kumsalimia lakini, alitueleza kuwa angerejea jana nchini,”alisema Minja.

Hata hivyo, bado haijajulikana sababu za kujiua, lakini baadhi ya ndugu zake wanasema ni kutokana na msongo wa mawazo.

Taarifa za kifo cha Mawalla anayemiliki kampuni kadhaa ikiwamo Kampuni ya uwakili ya Mawalla Advocates, kimeshtua wengi akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema taifa limepoteza kijana mwenye maono, akili na mjasiriamali aliyetajirika bila kuiba.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Nyaga. Licha ya udogo wake kiumri, lakini alikuwa mshauri wangu kwenye mambo mengi kiuchumi, kibiashara na kijamii. Nyaga alikuwa kiongozi wa jamii asiye na mipaka katika huduma tofauti na wafanyabiashara wengi nchini walishirikiana naye,” alisema Mbowe.

Mawalla ambaye ni mtoto wa wakili wa kwanza wa kujitegemea nchini, Juma Mawalla alikuwa jijini Nairobi kwa matibabu ya kupungaza sumu mwilini kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za shinikizo la damu kwa muda mrefu.

Wakati kifo hicho cha ghafla cha Mawalla kikitokea, Jiji la Arusha pia linaomboleza kifo kingine cha ghafla cha mfanyabiashara maarufu wa madini, Henry Nyiti kilichotokea mkoani Morogoro.

Nyiti ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Interstate yenye makao yake makuu eneo la Tengeru, wilayani Arumeru alifariki usiku wa kuamkia juzi akiwa Mahenge alikokwenda kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini na anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake eneo la Akheri, Arumeru keshokutwa Jumanne.

Akimzungumzia wakili Mawalla, Mbowe alisema mchango wake kwa maendeleo ya jamii hautasahaulika hasa kutokana na kujitolea kuendeleza taaluma ya uwakili kwa kudhamini tuzo ya wakili kijana kwa kutoa dola 5,000 kila mwaka kumsomesha mshindi wa tuzo hiyo.

Mbowe ambaye mwezi uliopita alipokea hati ya kiwanja chenye thamani ya Sh500 milioni iliyotolewa kwa Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF) na wakili huyo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, alipendekeza hospitali hiyo iitwe Nyaga Mawalla Memorial Hospital kama njia ya kumuenzi.

Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema ambaye ndiye mwanzilishi wa taasisi ya ArDF, alimwelezea Mawalla kama kiongozi, tajiri na kijana aliyetumia akili, nguvu na rasilimali zake akishirikiana na viongozi wote bila kujali tofauti zao kiitikadi.

“ArDF tutauenzi na kuuthamini utu uliouonyesha Mawalla kwa kukamilisha ndoto ya kuwa na hospitali ya kisasa ya mama na watoto ili kuokoa maisha ya kundi hilo linapoteza maisha kwa kukosa huduma bora na sahihi,” alisema Lema.

Fred Lowassa, mtoto wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa alimwelezea wakili Mawalla kama kijana aliyeonyesha nidhamu tangu akiwa shule na aliendelea nayo hadi kwenye kazi na shughuli za kiuchumi kiasi cha kufanikiwa na kutumia utajiri wake kusaidia jamii. “Kifo hiki ni pigo siyo tu kwa Arusha bali taifa zima la Tanzania.”

Mchango wa Mawalla kwenye kuendeleza sekta ya elimu, hasa sheria umetukuka ndiyo maana alijitolea hata kufundisha bila malipo kwenye vyuo vikuu kadhaa nchini,” alisema Lowassa.

Pamoja na kujitolea kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo, Mawalla pia alikuwa mfadhili wa watoto kadhaa wenye mahitaji maalumu ambapo hadi mauti yanamkuta, alikuwa akisomesha wanafunzi kadhaa katika ngazi mbalimbali kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.

Nyumbani kwake anaishi na zaidi ya watoto saba ambao amewachukua kutoka sehemu na familia mbalimbali nchini anaowalea, kuwahudumia na kuwasomesha kama watoto wake wa kuwazaa.

Ingawa haikuweza kujulikana haraka kutokana watu walio karibu naye wote kudaiwa kuwa jijini Nairobi, mwili wa wakili huyo unatarajiwa kuletwa nchini kati ya leo na kesho na kupelekwa moja kwa moja katika chumba cha kuhifadhi maiti cha KCMC, mjini Moshi kusubiri maziko yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwao Marangu.

KESI YA LWAKATARE: TUNDU LISU AMLAUMU "ISSA MICHUZI" NA " MWIGULU NCHEMBA"




Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu akiongea na wanahabari (hawapo pichani).
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu leo amefanya mkutano wa wanahabari. Katika mkutano huo, Lissu ameongea yafuatayo:

1. Atafungua kesi Mahakama kuu kuiomba iiamuru Mahakama ya Kisutu kuendelea kusikiliza kesi ya awali iliyofutwa na DPP katika kesi inayomhusu Lwakatare kwani DPP amevuka mipaka yake inayomruhusu kufuta kesi na isitoshe kesi aliyofungua ni ile ile hivyo Mahakama iamuru shauri la awali liendelee.

2. Kuhusu video iliyoonyeshwa kwenye mitandao Lissu anasema kuna mashaka makubwa sana kuhusiana na video ile na kisheria kesi hiyo ikifika mahakamani haitachukua hata nusu saa ataibuka mshindi.
Lissu anasema
- Hakuna mtu anayepanga mauaji katika hadhara mahali ambapo watu wanapitapita kama inavyoonekana kwenye video ile.

-Lwakatare kama alirekodiwa basi lazima ielezwe je ilikuwa ni kwa hiari yake kama si hivyo ni makosa

-Issa Michuzi Mpiga picha wa Rais alikuwa akipongezana na watu wa Ikulu wenzake kuwa TISS (Usalama wa Taifa) wamefanya kazi nzuri kwa kurekodi ile video. Kisheria usalama wa taifa hawatakiwi wala hawaruhusiwi kurekodi au kuvifanyia ushushu vyama vya siasa kwa maslahi ya Chama tawala.

-Ludovick baada ya kukutana na Lwakatale tarehe 28 Desemba mwaka jana saa 5 muda mfupi baadaye yaani saa 5:59 alimpigia simuMwigulu Nchemba kwa kutumia namba ya simu ya Mwigulu ambayo ameiandikisha kwenye kumbukumbu na vitabu vya Bunge Lissu anadai wana rekodi ya mazungumzo yao.

-Siku iliyofuata tarehe 29 Desemba mwaka jana akiwa kwenye kipindi cha Tuongee asubuhi cha Star TV alidai ana mkanda wa video unaowaonyesha CHADEMA wakipanga mauaji.

-Pia amedai itabidi waambiwe video hiyo imerekodiwa studio gani, maneno gani yameondolewa na yapi yameongezwa.

Anamalizia kwa kusema walianza kwa kusema CHADEMA ni chama cha familia wakashindwa, wakasema ni chama cha wachaga wakashindwa, wakesema ni chama cha wakatoliki wakashindwa, wakasema ni chama cha wakristo wakashindwa, wakasema ni chama cha ukanda wakashindwa leo wanasema ni chama cha kigaidi WATASHINDWA.

(Picha / Habari na Kurugenzi Ya Habari Chadema)

CHADEMA yafichua siri video ya Lwakatare


SAKATA la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, kufunguliwa kesi ya ugadi akidaiwa kupanga mikakati ya kudhuru watu, limechukua sura mpya baada ya chama hicho kudai kunasa mawasiliano ya watu kinaowatuhumu kuandaa video hiyo.
Pia CHADEMA imesema kuwa mawakili wake wamepeleka hati ya dharura katika Mahakama Kuu wakiiomba iingilie kati kwa kuitisha mafaili yote mawili ya kesi hiyo inayomkabili Lwakatare na mwenzake Ludovick Joseph.
Lwakatare alikamatwa Machi 13 mwaka huu na kuhojiwa kwa siku nne kisha kufikishwa mahakamani Machi 18 na kufunguliwa kesi namba 37/2013 yenye mashtaka manne huku Ludovick akisomewa mashtaka matatu.
Akizungunza na waandishi wa habari jana makao makuu ya CHADEMA, mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, alidai kuwa wamenasa mawasiliano ya watu mbalimbali wanaowahisi kuhusika kurekodi video hiyo.

Lissu aliwataja watu hao kuwa ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky, Ludovick na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Mwigullu Nchemba.
Alifafanua kuwa Desemba 27 siku moja kabla ya video hiyo haijarekodiwa kulikuwa na mawasilano ya simu kutoka kwa Msacky kwenda kwa Lwakatare akimuulizia sehemu alipo.
Alisema katika mawasiliano hayo, Msacky anayetajwa kudhuriwa na mkakati huo alimpigia simu Lwakatare na kumuulizia mahali alipo ambapo alijibiwa kuwa alikuwa yuko njiani kurejea Dar es Salaam.

Lissu ambaye pia ni mmoja wa jopo la mawakili wanaomtete Lwakatare, aliongeza kuwa Desemba 28, Ludovick alifika nyumbani kwa Lwakatare siku ambayo video hiyo ilirekodiwa saa 11:59.
Aliongeza kuwa kulikuwa na mawasiliano baina ya Ludovick na Nchemba kwa kutumia namba za simu ya Nchemba inayoonekana katika kitabu cha Bunge.
Lissu alidai kuwa baada ya mawasiliano hayo kati ya Desemba 29 mwaka jana na Januari 2 mwaka huu, Nchemba alinukuriwa katika kituo cha televisheni akisema anayo video inayowaonyesha viongozi wa CHADEMA wakipanga njama za mauaji.
“Tumegundua mengi katika haya na kama tutafika mahakamani jaji au hakimu atakayekuwa anasikiliza tukiwa na hoja zetu atamaliza kesi hii ndani ya saa zisizozidi tatu,” aliongeza Lissu.
Alipotafutwa Msacky kwa simu yake ya kiganjani ili afafanue madai hayo, alikataa akidai kuwa kesi iko mahakamani.
Kuhusu kupeleka hati ya dharura kuiomba mahakama iitishe mafaili yote mawili na kutengua uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka wa kumfutia Lwakatare mashtaka uliotolewa juzi, Lissu alisema wanatambua mamlaka ya kiongozi huyo katika kufungua na kuiondoa kesi mahakamani.
Alisema lengo ni kulinda maslahi ya taifa au kuboresha utendaji wa haki, suala alilodai halikufanyika katika dhamira nzima ya kufuta kesi ya kwanza ya Lwakatare.
“Tumekaa jopo la mawakili watano; tumeiomba mahakama kuu iingilie kati na kuitisha mafaili yote mawili ya kesi hii na kisha ijiridhishe kama sababu ya kufutwa kwa kesi ya kwanza ni kwa ajili ya maslahi ya taifa,” alisema.
Alisema maombi mengine katika hati hiyo ni pamoja na kuiomba mahakama ichunguze ili kuona kama haki imetendeka kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, pia wameiomba ifute hati ya kufutiwa mashtaka kwa Lwakatare na ifute amri ya kumaliza kesi hiyo.
Pia alieleza kuwa wameiomba mahakama kuu iiamuru mahakama ya hakimu mkazi kisutu kuendelea na kesi ya awali iliyofunguliwa Machi 18 mwaka huu na pia itamke kuwa kilichofanywa na mawakili wa serikali ni kuingilia uhuru wa mahakama wa kufanya uamuzi.
Aliongeza katika kesi ya awali walihoji uwepo wa hati ya ridhaa ya DPP juu ya mteja wao kushtakiwa kwa sheria ya kupambana na ugaidi na wakaonyeshwa makaratasi yasiyokuwa na nembo yoyote ya taifa, hali iliyowafanya wahoji na kumuomba hakimu aifute kesi hiyo ombi lililokuwa linatarajiwa kutolewa uamuzi juzi.

Lissu alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya ugaidi ili kosa liwe la kigaidi lazima maelezo ya kosa hilo yaonyeshe kuwepo kwa malengo ya ugaidi hali aliyosema katika mashtaka yote mawili suala hilo halionekani.

Chanzo: Tanzania Daima