Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mh Freeman Mbowe, ambe pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni akihutubia katika hafla ya makabidhiano ya kiwanja alichoahidiwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mh Godbless Lema na Kampuni ya Mawalla Advocates na Mawalla Trust ya Jijini Arusha leo asubuhi.
Hafla hiyo fupi ilifanyika katika kiwanja hicho chenye ukubwa wa ekari tatu eneo la Burka, nje kidogo ya Jiji. Kiwanja hicho kinathamani ya Jumla ya shilingi milioni 480 (USD 300,000).
Mbowe alisifu jitihada za Mbunge Lema kupigania maendelo ya watanzania, na pia akakumbushia ulazima wa nafasi tano za madiwani kuzibwa mapema iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti wa ArDF (Mfuko wa Mbunge Lema kwa Maendeleo ya Arusha),Bw Elifuraa alisema mradi huo wa hospitali ya mama na mtoto utasimamiwa kwa karibu na taasisi hiyo lakini haitakuwa jukumu lake pekee bali wananchi wote bila kujali itikadi zao.
Elifuraa alisema tayari mchora ramani amekwishapatikana na kupatiwa jukumu la kuandaa michoro lakini pia ArDF wanafanya mawasiliano na madaktari bingwa ili waweze kutoa mawazo yao ili jengo liwe la kisasa zaidi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Arusha Mjini Mh Godbless Lema alisema kwamba tukio hili la leo ni faraja sana kwake na ni jibu kwa wote walioandika ama kuzungumza mabaya dhidi yake siku za nyumba kwamba alishakabidhiwa viwanja hivyo na kuviuza, kitu amcho amedai leo imedhihirika ukweli na uongo ni upi.
Lema ameahidi kutimiza kila ahadi aliyowaahidi watanzania hususani wakazi wa Arusha na kwa kuazna na hospitiali ya kina mama na watoto amedai mipango iliyopo ni mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu jengo la Utawala la hospitali hiyo litakuwa tayari.