KWA mujibu wa mashuhuda wa ajali iliyotokea leo asubuhi Jijini Arusha, inakadiriwa zaidi ya watu 18 wamepoteza maisha kufuatia kufukiwa na gema la mchanga/moram wakati wakichimba na kupakia kwenye malori.
Ajali hiyo mbaya imetokea katika machimbo ya moram nje kidogo ya Jiji eneo jirani na Moshono-Kiserian ambapo vijana hao wanaokadiriwa kufikia idadi hiyo walikuwa wakipakia moram kwenye magari mawili, moja ni Fuso na lingine kubwa zaidi (tani 18) na yote mawili yamefukiwa kabisa na kifusi.
Shuhuda mmoja wa ajali ambae pia ni mchimbaji ameieleza Blog hii kwamba kwa kawaida gari ndogo kama Fuso hupakiwa na watu 7, na hiyo kubwa huwa na watu 12 bila kuhesabu dereva na utingo.
Blog hii iliweza kushuhudia sehemu ndogo sana ya Fuso ikionekana lakini gari nyingine ilikua imefukiwa kabisa na kupondeka vibaya.
Miongoni wa waliofikwa na mauti ni pamoja na madereva wa magari hayo. taarifa za eneo la tukio zinaeleza utingo mmoja ameokolewa akiwa amejeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali lakini dereva wake amefariki dunia.
Katika eneo la ajali hali ni ya simanzi na vilio toka kwa kina mama huku baadhi wa wababa na marafiki na ndugu wa jamaa waliofukiwa wakishindwa kujizuia na kuangua kilio.
Meya wa Manispaa Mh Gaudence Lyimo pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini Mh Godbless Lema ni miongoni mwa viongozi wakubwa waliofika eneo la ajali kusaidiana na kikosi cha Jeshi la Wananchi kufanya uokozi.
Blogu hii ilishuhudia pia Wachina wakipeleka moja ya mashine zao (Excavator) kuongeza nguvu katika kusaidia kufukua miili ya watu hao iliyonaswa na kifusi hicho.
Tunaomba radhi kwa ubora hafifu wa picha hizi….