CHADEMA:HUJUMA:Yatangaza kukamata mtandao wa kutawanya fedha kuhonga


Mkurugenzi Wa Sheria na Haki za Binadamu Chadema
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimebaini kuwapo kwa njama zinazofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya vyombo vingine vya usalama na ujasusi wa kutengeneza ushahidi wa uwongo kwa ajili ya kuutumia mahakamani katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama hicho, Wilfred Lwakatare.

Pia kimesema kuna baadhi ya vyombo vya habari nchini vinatumiwa kukichafua na kukipaka matope ili kionekane kuwa ni chama cha fujo na kigaidi ili Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, akifutie usajili.

Kauli hiyo ilitolewa na Chadema kupitia Mkurugenzi wake wa Mambo ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

Alisema mbali na hayo, pia kuna baadhi ya vijana wa Chadema wa Idara ya Ulinzi na Usalama wanaopewa fedha na kuahidiwa kufundishwa namna ya kuzungumza katika kesi ya Lwakatare mahakamani.

Lissu alisema mpaka sasa vijana hao wameshapewa Sh. 400,000 ili wakubali kwenda kufundishwa jinsi ya kuzungumza mahakamani kuwa Chadema ni chama cha kigaidi na 
Lwakatare alipanga mikakati ya kigaidi.

“Awali walipewa 400,000, wakapewa tena 300,000, pia wakapewa 35,000 mara mbili. Na pesa zote hizo walikuwa wanapewa kwa njia ya M-Pesa,” alisema Lissu.

Hata hivyo, Lissu alikataa kuwataja vijana hao wa Chadema waliopewa fedha hizo.
Lakini akamtaja mmoja wa wafanyakazi wa chama hicho aliyekuwa makao makuu (jina tunalihifadhi) na alikwisha kufukuzwa kazi kwa kukosa uaminifu, kuwa alikuwa anawafuata na kuwapa fedha hizo.

Lissu alisema mfanyakazi huyo ndiye anayeratibu mpango wote kati ya Jeshi la Polisi na vijana hao wa Chadema kwa kuwarubuni kwa fedha.

Alisema vikao baina ya vijana hao wa Chadema na mfanyakazi huyo vimewahi kufanyika mara kadhaa katika moja ya hoteli maarufu nchini juu ya mambo ya kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari au mahakamani kwenye kesi ya Lwakatare.

“Hayo yote yanayofanyika kufundisha watu au kupika ushahidi kwa mujibu wa sheria ya Tanzania ni kinyume cha sheria na ni kosa la jinai,” alisema Lissu.

Aidha, Lissu alizungumzia uhusiano uliokuwapo baina ya Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Mwigulu Nchemba,  na mmoja wa watuhumiwa katika kesi moja iliyoko mahakamani.

Alisema Januari 14, mwaka huu, saa 11:47, mtuhumiwa huyo alipokea Sh. 50,000 kwa M-pesa kutoka kwa Nchemba, na siku ambayo Lwatakare na mtuhumiwa huyo walikutana kwa mazungumzo yanayoaminiwa kuwa alikuwa anapanga njama za kigaidi.

Alisema Nchemba kupitia simu yake ya mkononi namba 0756008888, alimtumia mtuhumiwa huyo kiasi hicho cha fedha na namba ya risiti 7UA511.

“Sasa swali la kujiuliza, Nchemba alimtumia mtuhumiwa kiasi hicho cha fedha kwa madhumuni gani? Je, ni zawadi kwa ajili ya mkanda wa video? Na ni siku ambayo mtuhumiwa alitoka kuongea na Lwakatare,” alisema Lissu.

Alisema Desemba 29, mwaka jana, Nchemba akiwa na mmoja wa viongozi wa Chadema Taifa (jina tunalihifadhi), katika kipindi runinga aliutangazia umma kuwa ana mkanda unaonyesha viongozi wa Chadema wakipanga mauaji, siku moja baada ya mkanda huo kurekodiwa.

Aliongeza hivi karibuni moja ya magazeti (siyo NIPASHE) lilimnukuu Nchemba akisema ‘aibuka’ na katika maelezo yake, Nchemba hajakanusha kama aliongea na mtuhumiwa kipindi cha nyuma.

Alisema kwa maelezo hayo, inaonyesha dhahiri kuwa kesi hiyo ilikuwa imetungwa.
Aliongeza kuwa Chadema imepata pia taarifa za mawasiliano baina ya mtuhumiwa huyo na watu wengine aliokuwa anawasiliana nao.

Alisema taarifa hizo zinaonyesha kabla ya tarehe hiyo (Desemba 28), aliwasiliana na mmoja wa waandishi wa habari waandamizi nchini (jina tunalo).

Lissu alisema njama hizo zinapangwa na baadhi ya watu wanaotaka Chadema isiaminike kwa wananchi.
“Kumekuwapo na misemo mingi. Mara Chadema ni chama cha Mtei na Mbowe, Chadema ni chama cha kaskazini, Chadema ni chama cha Wachagga. Na sasa wanasema Chadema ni chama cha kigaidi. Hiyo yote ni kutaka kukiua chama,” alisema Lissu.

Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu, alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia madai hayo, alisema suala hilo lipo mahakamani kwa sasa na kwamba, kama Chadema wanadhani kuna njama zimepangwa itafahamika mahakamani.

“Siwezi kujibu hilo. Ila kama Chadema wanaona kama suala hilo ni la kusingiziwa au ni njama zimepangwa kukichafua chama, itafahamika huko huko mahakamani,” alisema Mngulu.
NIPASHE lilimtafuta Nchemba, ambaye alisema Chadema hawana hoja ya msingi ya kumsingizia yeye kuhusika katika tukio hilo bali wanatapatapa kupata visingizio.

Alidai kuwa wahusika wakuu waliokuwa wanapanga tukio hilo ni viongozi waandamizi wa Chadema.

Aliongeza kuwa mkanda wa video unaonyesha kila kitu walichokuwa wanapanga kupitia kiongozi huyo.

"Mimi sihusiki na chochote na tukio hilo wala upangaji, huko ni kutapatapa waende katika hoja," alisisitiza.
CHANZO: NIPASHE