TUME YA PINDA KIINI MACHO TU:




KAMA ilivyotarajiwa, wananchi wengi wamebeza hatua ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ya kuunda tume ya kuchunguza matukio mabaya ya kidato cha nne kwa mwaka 2012. Pamoja na kuona hatua hiyo ya Waziri Mkuu kama kiinimacho tu, wamesema haitakuja na jambo jipya kwa kuwa huko nyuma tume za aina hiyo ziliundwa siyo kwa lengo la kutatua matatizo, bali kwa kufunika kombe ili mwanaharamu apite.

Kwa maana hiyo, Serikali imekuwa ikiunda tume nyingi ikiwa kama njia ya kupata muda wa kupumua baada ya kutokea matukio mabaya kama hilo la mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana na kutangazwa wiki iliyopita.
Kama ilivyotokea katika tukio hilo la wiki iliyopita, wananchi wamekuwa wakikasirishwa na kughadhabishwa na matukio ambayo wanaona yanasababishwa na Serikali na madhara yake kuwa mwiba mkali kwa wananchi.

Hata baada ya kuunda tume hizo, Serikali imekuwa haiyafanyii kazi mapendekezo yaliyomo katika ripoti za tume hizo. Mara nyingi Serikali imekuwa ikizikalia ripoti hizo na kuzifanya siri. Wakati mwingine imekuwa ikitangaza baadhi ya vipengele inavyoona havielekezi lawama kwa Serikali moja kwa moja au kuwa na nguvu zinazoweza kuchochea hasira kali za wananchi dhidi yake, hivyo kuilazimisha kuwajibika.

Ndiyo maana wengi wanadhani Tume ya Pinda ni kiinimacho tu na kwamba hapakuwapo sababu ya kuunda chombo hicho kitakachofuja fedha za walipa kodi wakati matatizo yaliyosababisha matokeo hayo ya aibu katika mtihani huo yako wazi kama ilivyo usiku na mchana.

Moja ya sababu zinazowafanya wananchi wakose imani na tume hiyo ni hatua ya Serikali ya kukataa kuwaweka kando viongozi wakuu wa wizara husika ili wapishe uchunguzi na kuiwezesha tume hiyo kutoa matokeo ya uhakika bila kuingiliwa na upande wowote kwa lengo la kuinusuru sekta ya elimu.

Wananchi wanazo sababu za msingi kwa kutokuwa na imani na tume zinazoundwa na Serikali. Mwaka 2004 aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye aliunda tume kuangalia matatizo katika sekta ya elimu. Tume nyingine iliundwa mwaka 2010.

Tume ya mwaka 2011 ilihusu Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa lengo la kuchunguza sababu za walimu kufeli katika vyuo vya ualimu. Tume hizo zilitoa ripoti, lakini Serikali haijawahi kutangaza matokeo au kuwaeleza wananchi juu ya hatua zilizochukuliwa.

Kwa jambo zito kama hilo la anguko la kihistoria katika mtihani wa kidato cha nne, wengi walitegemea kwamba Rais Jakaya Kikwete kwanza angetangaza hali hiyo kama janga la kitaifa.

Hiyo ingefuatiwa kwa karibu na kuunda tume ya kuchunguza tukio hilo na kuwaweka kando viongozi wakuu wa wizara husika, akiwamo Waziri Shukuru Kawambwa ili kupisha uchunguzi.
Lakini tunachoshuhudia hivi sasa ni mwendelezo wa utamaduni wa kulindana, licha ya ukweli kwamba kiwango cha elimu kimekuwa kikiporomoka mwaka hadi mwaka chini ya uongozi wa Waziri Kawambwa.

Hakuna asiyejua kwamba mfumo wa elimu katika nchi yetu ulikufa miaka mingi iliyopita na haikuwa rahisi kuufufua kutokana na wanasiasa kufanya elimu kuwa suala la kisiasa. Ujenzi wa shule za kata, kwa mfano lilikuwa jambo la kheri, ingawa ulifanyika kwa kukurupuka ili kutimiza malengo ya kisiasa ya chama fulani.

Ni matumaini yetu kwamba Tume ya Pinda haitafanya kazi kisiasa, bali itatoa majibu hadharani jinsi ya kuusuka upya mfumo wetu wa elimu ambao umevurugika.