Bashe anusurika kutekwa



Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd
WIMBI la viongozi wakuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, kuendelea kuwindwa na watu wasiofahamika, limeendelea kushika kasi, baada ya usiku wa kumkia jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Hussein Bashe, kunusurika kutekwa. Tukio hilo, lilitokea juzi usiku wakati Bashe alipokuwa akitoka ofisini kwake Sinza Kijiweni, akielekea nyumbani kwake Mbezi.

Akizungumzia tukio hilo, Bashe alisema wakati anaondoka ofisini kwake kwa gari lake, alianza kufuatiliwa kwa nyuma na magari mawili, likiwamo aina ya NOA ambalo hata hivyo hakufanikiwa kujua lilikuwa na watu wangapi.

“Kama kawaida nilishinda ofisini kwa ajili ya majukumu yangu ya kazi na muda wa kutoka ulipowadia, niliondoka kurudi nyumbani.

“Awali wakati navuka geti la pale ofisini, sikuwa na shaka yoyote, lakini kadri nilivyozidi kuendelea na safari yangu, niliona nyuma nafuatiliwa na magari mawili ambayo yalikuwa yakiendeshwa kwa tahadhari.

“Nilipofika Mwenge ile NOA ilikuwa bado iko nyuma yangu, sasa nikaanza kupatwa na wasiwasi, nikajua hapa kuna jambo.

“Moyoni niliendelea kumuomba Mungu, huku nikijiuliza maswali mengi hawa jamaa ni akina nani, kwa kweli sikupata jibu zuri.

“Nilipofika Mbezi, niliona yale magari yanazidi kunisogelea, kwa hiyo, nikaamua kuongeza kasi na wao wakazidi kuja tu.

“Wakati niko Mbezi jirani na njia panda ya kwenda kwangu, gari moja lilinipita kwa kasi na kuendelea mbele.

“Unajua kuelekea kwangu pale kuna barabara kama tatu ambazo zote unaweza kuzitumia na zikakufikisha hadi nyumbani kwangu,” alisema Bashe na kuongeza:

“Nilichokifanya nilipita barabara ya kwanza na wao wakapita barabara ya pili na ghafla nilikutana nao uso kwa uso, wakati huo naelekea kwangu na kibaya zaidi, gari lao walizima taa kubwa na kuacha ndogo.

“Walivyona gari langu, walinipiga taa kuashiria wanakata kona, lakini cha ajabu walinifuata nyuma na hapo nikaanza kujua sasa nafuatiliwa.

“Nilichokifanya sikwenda nyumbani moja kwa moja, bali niliamua kupaki gari kwenye grosari moja iliyoko jirani na kwangu.

“Baadaye niliamua kuondoka ili niwazunguke kwa nyuma nisome namba za gari lao, lakini sikufanikiwa kwa sababu taa za nyuma zilikuwa zimezimwa,” alisema Bashe.

Kwa mujibu wa Bashe, baadaye aliingia nyumbani kwake na kuwakuta wageni ambao alikaa nao hadi saa sita usiku baada ya kuwasimulia tukio lilivyokuwa.

“Sasa basi, wakati jamaa zangu hao wanaondoka kurudi kwao, walikuta lile gari pale pale njiani, wakanipigia simu, kwamba lile gari nililowasimulia linawafuatilia.

“Nikawaambia wageuze gari lao ili wasome namba, lakini hawakufanikiwa hata kidogo kwa sababu wale jamaa walishtuka na kuamua kutimua.

“Kwa hiyo, nilichokifanya nilikwenda pale Polisi Kawe na kutoa taarifa ambapo nilipewa RB yenye namba KW/RB/2899/2013,” alisema.

Machi 6, mwaka huu, Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, alitekwa na kuteswa na watu wasiofahamika.

Katika tukio hilo, Kibanda alitobolewa jicho la kushoto, alipigwa kichwani na kitu chenye ncha kali na kunyofolewa kucha. Kwa sasa yuko nchini Afrika Kusini ambako anaendelea na matibabu.