RAIS KIKWETE AENDA KUTOA POLE KWA FAMILIA YA ASKARI ALIYEKUFA KWA AJALI BARABARANI

Taarifa tulizozipata zinaeleza kuwa yule dereva aliyemgonga askari polisi wa usalama barabarani WP 2493 CPL-Elikiza Lokisa Nko na kutokomea, amekamatwa juzi usiku masaa kadhaa baada ya kupoteza uhai wa askari huyo maeneo ya Bamaga mapema jana mchana.

Kwa Mujibu wa Mkuu wa Kikosi cha Polisi cha Usalama barabarani nchini, Kamanda Mohamed Mpinga alisema jana kuwa gari lilohusika kwenye ajali hiyo aina ya Landlover Discovery rangi nyeusi limepatikana likiwa limefichwa maeneo ya Tabata dampo jijini Dar.

Kupatikana kwa gari hilo kumekuja baada ya Polisi kufuatilia na kujua mmiliki wa gari hilo kuwa ni kanisa la TAG chini ya Mchungaji Wambura, ambaye kwa ushirikiano alioutoa dereva aliyetambuliwa kama Jackson Stephen, alijulikana na hatimaye kupatikana

Kamanda Mpiga alitoa taarifa hiyo mbele ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete jana jioni nyumbani kwa Marehemu hukoUnunio kiasi cha kilomita 25 hivi Kaskazini mwa jiji la Dar.

Rais Kikwete pamoja na uongozi wa juu wa jeshi la polisi walifika kuhani msiba huo nyumbani kwa marehemu ambaye ameacha Mume na watoto watatu. Mume wa marehemu pia ni askari polisi.

Pichani juu Rais Kikwete akimfariji mume wa marehemu na watoto wake pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Saidi Mwema.