ULINZI MKALI SHEREHE YA KUTAWAZWA KWA PAPA FRANCIS 1 JIJINI ROME.

Papa Francis akisalimiana na Rais wa Argentina, Cristina Fernandez de Kirchner alipowasili Vatican, jana kuhudhuria sherehe za kutawazwa kwa mkuu huyo wa Kanisa Katoliki zitakazofanyika leo. Picha na AFP.


Vatican City. Ulinzi mkali umeandaliwa kwa viongozi mbalimbali wa kiserikali na wale wa kidini duniani waliowasili jijini Vatican, kwa misa maalumu ya kutawazwa kwa Papa Francis leo.


Waumini na wageni milioni moja akiwamo Balozi wa Tanzania nchini Italia, Dk James Msekela, wanatarajiwa kuhudhuria misa hiyo itakayofanyika kwenye Viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.


Baada ya Papa Francis kutawazwa, ataanza rasmi kazi ngumu ya kuliongoza Kanisa Katoliki lenye waumini wengi na ambalo limekumbwa na mizozo kadhaa ikiwamo ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya makasisi.


Kiongozi huyo alichaguliwa Jumatano iliyopita kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Papa Benedict XVI, aliyejiuzulu Februari 28, mwaka huu.