Precision Air imepigwa marufuku Zanzibar

Ndege ya shirika la ndege la Precision ikiwa angani Zanzibar,Tanzania
SHIRIKA la Ndege la Precision Air inayofanya safari zake nchini Tanzania na nchi jirani ya Kenya imepigwa marufuku kufanya safari zake na kutua katika Uwanja wa Kimataifa ya Zanzibar.

Precision Air imekumbana na balaa hilo baada Mamlaka ya Mapato ya Zanzibar (ZRB), kutangaza amri ya kuzuia kutua na kuruka kutokana na kutolipa zaidi ya Sh bilioni 37.2 zinazotokana na malimbikizo ya malipo ya ada ya huduma ya uwanja wa ndege.

Kamishna wa Bodi ya Mapato ya Zanzibar, Abdi Faki, alitangaza kuifungia Precision kufanya safari zake visiwani humo kutokana na malimbikizo hayo ya madeni inayodaiwa. Akizungumzia suala hilo Faki alisema, “Chini ya kifungu cha 43(1) cha taratibu na udhibiti wa kodi cha mwaka 2009, mimi Abdi Faki, Kamishna wa Bodi ya Mapato ninatoa amri ya kuzuia kuruka na kutua kwa ndege za kampuni ya Precision Air Service Co. Ltd kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kuanzia saa saba usiku wa Aprili 25 mpaka hapo watakapolipa fedha hizo.”

Amri hiyo iliyosainiwa na Faki April 25 mwaka huu na utekelezaji wake kuanza mara moja pia iliambatana na agizo la kufungwa kwa ofisi za shirika hilo endepo watashindwa kulipa deni hilo. Faki alisema kuwa Precision Air Service Co. Ltd, imeshindwa na kupuuzia kulipa deni la zaidi ya Sh milioni 144.8 na zaidi ya dola za Marekani 347,066 (zaidi ya Sh milioni 520.6), kama malipo ya makato ya huduma za viwanja na usalama kwa miezi mitatu tangu Januari hadi Machi mwaka huu. "Precision Air imeshindwa kulipa zaidi ya Sh milioni 70.5 na zaidi ya dola za Marekani milioni 1.6 (zaidi ya Sh bilioni 2.5), kama fedha za adhabu kutokana na ucheleweshwaji wa malipo kuanzia Februari hadi Agosti mwaka 2012, ZRB imekuwa ikiwakumbusha Precision Air Service Co. Ltd mara kwa mara ili kulipa deni hilo, lakini wameshindwa na kupuuzia suala hilo. Sheria inatutaka kufuata utaratibu wa kukusanya na kulinda mapato ya Serikali,” alifafanua Faki.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara cha Precision Air, Patrick Ndekana, alipoulizwa alisema sio kweli kuwa ndege zao zimefungiwa. “Sio kweli kuwa ndege zetu zimezuiliwa kutua na kuruka Zanzibar, mpaka muda huu ninaozungumza nawe (saa 11 jioni) kuna ndege yetu inajiandaa kuruka kutoka Zanzibar,” alisema Ndekana. Kuhusu kudaiwa zaidi ya bilioni 37.2, Ndekana alisema hana taarifa na kuongeza kuwa hilo ni suala la watu wa fedha na kuahidi kulitolea ufafanuzi zaidi